SERIKALI inakusudia kuajiri watumishi wapya wa umma 52,436 katika mwaka ujao wa fedha. Aidha, madaktari wapya 258 waliokuwa waende kufanya kazi nchini Kenya, lakini wakakwama kutokana na kuwekewa pingamizi la kimahakama na wenzao wao huko na hivyo Rais, Dk John Magufuli kuamuru waajiriwe mara moja nchini, watarajiwa kuanza kazi keshokutwa Jumatatu.
Hayo yalisemwa bungeni juzi usiku na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki alipokuwa anatoa ufafanuzi wa lini Serikali itaendelea kuajiri watumishi wa kada nyingine, kama ilivyoulizwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Lupembe (CCM).
“Azma ya serikali, kwanza kabisa hatuwezi kuajiri wananchi wote, tumekuwa tukisikia hapa wahitimu hawana ajira, wengine wanaendesha bodaboda… tunapopanga idadi ya watumishi wa kuajiriwa, tunaangalia mambo mengi, kuanzia mahitaji, vipaumbele hadi uwezo wa kibajeti.
“Tayari tumeshaanza kutoa vibali vya ajira zaidi ya watu 9,700 na tutaendelea kufanya hivyo, na hivi karibuni Rais amebariki kuajiriwa kwa madaktari wapya 258 na Jumatatu (keshokutwa) wanaripoti kazini.
Tutaendelea kuajiri na wataalamu wa kada nyingine, kabla ya kumalizika kwa mwaka huu wa fedha mwezi Juni tutakuwa tumejiajiri kwa idadi tutakayoipanga kwa awamu, na katika mwaka ujao wa fedha tutaendelea kuajiri watumishi wengine wa umma zaidi ya 52,436,” alisema.
Hata hivyo, alisisitiza Serikali itahakikisha hairudii makosa ya kuajiri watumishi hewa, wasio na sifa na weledi unaohitajika. Alisema kwa kiasi kikubwa uhakiki wa watumishi wa umma kwa ujumla umekwisha, lakini kazi hiyo ni endelevu, kwani serikali itaendelea kufanya hivyo mara kwa mara.
Alisema matunda ya uhakiki wa watumishi wa umma umebaini watumishi hewa 19,708 na ambao wameshaondolewa katika orodha ya mishahara ya watumishi wa umma. “Hawa wangeachwa, Serikali ingekuwa inapoteza kiasi cha Sh bilioni 19.8 kila mwezi, lakini fedha hizi zimeokolewa kupitia uhakiki wa watumishi wa umma.
Tunafanya haya kwa nia njema. Mathalani tusingewatoa hawa, si wangeziba nafasi za ajira za wengine na fedha ngapi zingepotea?” alihoji. Alisisitiza kuwa, wizara hiyo itaendelea kutimiza majukumu yake kwa vitendo ili kurejesha nidhamu ya serikali na utumishi wa umma kwa kuongeza uwazi na kusimamia sheria, kanuni na taratibu za uwajibikaji wa viongozi wa watumishi wa umma ili wawajibike kwa wananchi ambao ndio wateja na waajiri wakuu wa watumishi wa umma.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene, akijibu hoja za wabunge, hasa la uhamisho wa watumishi wakiwemo wanandoa wanaotenganishwa, alikemea tabia ya maofisa watumishi kuzuia wenye ndoa kuhama kutoka kituo kimoja cha kazi kwa lengo la kuwafuata wenzao.
Alisema kuwazuia ni kuwanyima haki ya msingi, na kuwaagiza wabunge katika maeneo yao wasaidia kusimamia haki za watumishi. Lazima sheria za utumishi zizingatiwe, walimu hawa au watumishi wanayo haki ya kutoka sehemu moja kwenda nyingine, lakini pia kuishi na wenza wao, lakini utadhani mtumishi anapoomba ni kama anasaidiwa, hapana ni haki yake ya msingi, waheshimiwa tusimamie haki za watumishi,” alisema Simbachawene
0 comments:
POST A COMMENT