WAZIRI Mkuu wa zamani wa Israel, Ehud Barak ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa jinsi inavyovitunza vivutio vyake vya utalii. Barak anayeongoza kundi la watalii zaidi ya 100 kutoka Israel ikiwamo familia yake, aliwasili nchini mapema wiki iliyopita kwa ajili ya utalii.
Walitembelea Makumbusho ya Olduvai Gorge na kueleza kufurahishwa kwake na jinsi Serikali inavyofanya katika kuhifadhi maeneo ya kihistoria kama Olduvai Gorge. Aidha, walitembelea Hifadhi za Taifa za Ngorongoro na Serengeti zilizoko katika Urithi wa Dunia, unaotambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Taifa la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Pascal Shelutete, alisema Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Israel alizuru pia Olduvai Gorge akiwa njiani kwenda Hifadhi ya Taifa ya Serengeti alikopokelewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani. Akiwa Olduvai Gorge ambayo ni moja ya eneo maarufu la masuala la kale katika Afrika Mashariki na linalotembelewa kwa kiasi kikubwa na watalii wakienda katika hifadhi za taifa za Ngorongoro na Serengeti, Barak alisema eneo hilo ni muhimu kutokana na uhusiano wake na binadamu wa kizazi cha sasa.
Akiwa na msafara wake waliwasili nchini Jumanne iliyopita wakitumia ndege ya Shirika la Ndege la Israel, na kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) walipokelewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe. Mapema mwezi huu, Balozi wa Israel nchini, Yahel Vilan alimtembelea Rais John Magufuli na kumueleza kuwa watalii wapatao 200 walikuwa wanatarajiwa kuitembelea nchi mwezi huu.
Tanzania na Israel zimeapa kudumisha uhusiano wake na ulipata nguvu zaidi baada ya uamuzi wa Tanzania kufungua ubalozi wake nchini Israel na kufunguliwa kwa kituo cha Israel cha utoaji viza jijini Dar es Salaam, Novemba mwaka jana. Sekta ya utalii itanufaika kutokana na hatua hizi. Kulingana na taarifa za kuaminika kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), idadi ya watalii kutoka Israel imeongezeka kutoka 3,007 mwaka 2011 hadi 14,754 mwaka 2015.
0 comments:
POST A COMMENT