WATANZANIA wameshukiwa na neema katika mwaka huu wa fedha kutokana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupanga kuunganisha mikoa yote nchini kwa kujenga barabara za lami na madaraja.
Bajeti hiyo ni ya neema pia kwa wakazi wa Dar es Salaam kutokana mkoa huo kupangiwa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kujenga barabara za lami nyingi, za viungio na za juu kwa ajili ya kupunguza msongamano wa magari jijini humo na katika majiji na mji mikubwa mingine.
Bajeti hiyo ya mwaka 2017/18 ya Sh trilioni 4.5 imeweka vipaumbele katika kukamilisha miradi inayoendelea, miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo kwa miaka mitano 2016/17 hadi 2020/21, kutekeleza ahadi za ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu 2015 na ahadi za viongozi wa serikali walizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka juzi.
Akisoma bungeni jana, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alisema, bajeti hiyo ya ukombozi kwa maana ya kuwa inalenga kuunganisha mitandao ya barabara nchini ambayo ni muhimu katika kujenga uchumi wa viwanda.
“Bajeti hiyo iliyotengwa katika sekta tatu za wizara hiyo, sekta ya ujenzi itatumia Sh trilioni 1.9 wakati sekta ya uchukuzi ambayo imeongoza kwa kuombewa fedha nyingi inaomba kupewa Sh trilioni 2.6 na mawasiliano Sh bilioni 18.1,” alisema.
Waziri huyo alisema, kati ya fedha hizo, trilioni 2.6 zilizoombwa kwa ajili ya sekta ya uchukuzi, kiasi cha Sh bilioni 900 zitatumika katika kujenga Reli ya Kati sehemu ya Dar es Salaam hadi Dodoma kwa kiwango cha standard gauge.
Profesa Mbarawa alisema, pia Sh bilioni 500 zitatumika katika kampuni ya ndege kwa ajili ya kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege tatu ambapo mbili za aina ya CS 300 zenye kubeba abiria 127 kila mmoja na moja ya masafa marefu aina ya Boieng 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 22.
Kuhusu Sekta ya ujenzi iliyotengewa Sh tril 1.9, Prof Mbarawa alisema Sh bilioni 12.8 zitatumika kwa ajili ya kufidia ili kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Dar es Salaam- Chalinze Km 144, ujenzi ambao utakuwa wa ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi (PPP).
Waziri Mbarawa alisema, kati ya fedha za sekta hiyo, Sh bilioni 30, zitatumika katika kujenga barabara za mikoani na madaraja ikilenga katika kuunganisha mikoa yote Tanzania kwa barabara za lami.
“Kazi zilizopangwa kutekelezwa ni ukarabati wa km 469.5 kwa kiwango cha changarawe, kujenga km 58.4 kwa kiwango cha lami na madaraja 12,” alisema. Alisema kati ya fedha hizo, Sh bilioni 46.9 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa flyover ya Tanzania, Interchange ya Ubungo pamoja na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kuboresha barabara za makutano.
“Barabara hizo ni iliyopo eneo la Kamata, Magomeni, Mwenge, Tabata/Mandela, Morocco, Buguruni, Makutano ya barabara za Kinondoni/ Ali Hassan Mwinyi na Kenyatta na Selander zinapokutana barabara ya Mwinyi na Umoja wa Mataifa (UN),” alisema.
Alisema, pia fedha hizo zitatumika katika kuboresha viwanja vya ndege kikiwamo cha Kimataifa cha Kilimanjaro kilichotengewa Sh bilioni 32.6 kwa ajili ya upanuzi wa barabra ya kuruka na kutua ndege.
“Fedha zitatumika kujenga maegesho ya ndege, barabara za viungio, jengo la abiria na ujenzi wa barabara mpya ya kiungio, usimikaji wa taa za kuongozea ndege na ujenzi wa mfumo mpya wa majitaka,” alisema.
Profesa Mbarawa alisema, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa cha JNIA umetengewa Sh blioni 35 kwa ajili ya kuendelea na ujenzi wa jengo jipya la abria terminal III na miundombinu yake.
Sekta ya mawasiliano imepata Sh bilioni 18.1 kidogo ukilinganisha na sekta nyingine mbili, fedha hizo pia zitatumika katika kuendeleza ujenzi wa mkongo wa Taifa hadi katika makao makuu ya wilaya zote nchini.
“Zitatumika pia katika ujenzi wa vituo viwili vya kutunza data kimoja Dodoma na kingine Zanzibar pamoja na kuwezesha uwekezaji wa viwanda nchini,” alisema. Kuhusu Mfuko wa Barabara, Waziri Mbarawa alisema, unatarajia kukusanya Sh bilioni 917.5 ambazo zitatumika katika kufanya matengenezo ya barabara nchini, katika fedha hizo sekta ya ujenzi imetengewa Sh bilioni 642.3 na ofisi ya Rais Tamisemi Sh bilioni 275.2.
Kati ya Sh bilioni 642.3 zilizotengwa, Sh bilioni 573.1 kwa ajili ya Tanroads na Sh bilioni 63.7 kwa ajili ya sekta ya ujenzi kufanya matengenezo ya barabara za wizarana Sh bilioni 5.52 kwa ajili ya uendeshaji wa Bodi ya Mfuko wa Barabara.
Mbarawa alisema, miradi ya barabara kuu itaendeshwa kutokana na fedha kutoka mfuko wa barabara, ambapo Sh bili 16.3 zimetengwa kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kilometa 3,624.8.
“Miradi ya barabara za mikoa imetengewa Sh bilioni 33.9 kutoka katika mfuko wa barabara, fedha hizo zitafanya kazi ya ukarabati wa barabara kilometa 688.3 kwa kiwango cha changarawe na kujenga kilometa 40.6 kwa kiwango cha lami na madaraja 12,” alisema.
Waziri Mbarawa alisema, jumla ya Sh milioni 573.1 kutoka mfuko wa barabara zitatumika kwa ajili ya matengenezo ya barabara kuu, barabara za mikoa, madaraja uendeshaji mizani, gharama za usimamizi na uendeshaji wa wakala wa barabara.
0 comments:
POST A COMMENT