
Katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani Miss Tanzania 2006 Wema
Sepetu ameshiriki kwa kupanda miti katika vyanzo vya maji vya Mbogo na
Nukutu katika milima ya Uluguru, Manispaa ya Morogoro.
Wema aliyeungana na Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Morogoro kupitia
CHADEMA, Devotha Minja, Diwani wa kata hiyo pamoja na wenyeviti wa
serikali za mitaa, wamefikia hatua hiyo kwa lengo la kuhifadhi vyanzo
vya maji ambavyo vimekuwa vikiharibiwa kwa kiasi kikubwa katika maeneo
hayo, hali inayotishia maisha ya viumbe pamoja na wakazi wanaotegemea
vyanzo hivyo.
Mrembo huyo ambaye pia msanii wa filamu nchini, amesema kuwa ameamua
kuunga mkono jitihada hizo za kuhifadhi vyanzo vya maji ili kuondoa kero
za maji ambazo wanawake hukumbana nazo, huku akitoa somo kuwa faida na
manufaa ya miti hiyo zitaonekana baadaye.
"Leo ni siku ya wanawake duniani, nikaonelea nijiunge na wanawake
wenzangu wa Mkoa wa Morogoro siku ya leo katika upandaji wa miti ambao
utakuja kuwa na tija kwetu na kupunguza kero kubwa inayotukabiri ya
maji, wote tunajua kuwa mwanamke ndiyo anakerwa zaidi katika upatikanaji
wa maji labda haittusaidia leo wala kesho lakini itakuja kusaidia
vizazi vyetu vya baadae". Amesem Wema Sepetu.
Wema ambaye hivi karibuni ametangaza kujiunga na CHADEMA akitokea CCM,
amesema ameongeza kuwa mazingira hayana itikadi wala vyama na kwamba
yanamgusa kila mtu hivyo yampasa kila mmoja kupanda miti ili kuweza
kulinda vyanzo vya maji.
Kwa upande wake Mbunge Devotha Minja ambaye kabla ya kuwa mbunge amekuwa
akiripoti habari nyingi kuhusiana na uharibifu wa mazingira kupitia
kazi yake ya uandishi wa habari, amesema ameamua kuchukua hatua kwa
vitendo kama kiongozi ili kuwa mfano kwa jamii nzima ya watanzania
hususani wakazi wa Morogoro, kuhusu umuhimu wa kuhifadhi mazingira na
vyanzo vya maji.
0 comments:
POST A COMMENT