WAKATI dunia ikiadhimisha Siku ya Wanawake leo, akina mama katika Kaunti
ya Mombasa, wametishia kuandamana uchi iwapo Naibu Gavana, Hazel
Katana, ataendelea kutoheshimiwa.
Wamesema Katana anakandamizwa na watu wasiojulikana walioko katika Serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa vile ni mwanamke.
Zaidi ya kina mama 200 waliandamana juzi katika bustani ya Uhuru wakimtaka Rais Uhuru Kenyatta aingilie kati siasa za Mombasa.
“Katika kipindi hiki cha kuelekea Siku ya Kimataifa ya Wanawake,
tutaandamana uchi wa mnyama, hatuwezi kukubali mama yetu aendelee
kudharauliwa eti ameiba viti vilivyozeeka. Kama alikuwa anataka kuiba
angeiba vitu vya maana,” alisema Asha Mwidani.
Walisema tangu mwenzao ajiengue kutoka Chama cha ODM na kwenda Jubilee
ambako atawania kiti cha useneta, amekuwa akikumbwa na misukosuko na
dharau kutoka kwa wafanyakazi wa kaunti kutokana na jinsia yake.
Wakibeba mabango yanayomtaja Katana, kina mama hao walisema wanasiasa wanawake wanapaswa kuheshimiwa na wanaume.
“Katana anapaswa kuheshimiwa kama viongozi wengine wa kiume. Kama gavana
hayupo, Katana anapaswa kuchukua nafasi yake ya usimamizi wa shughuli
za kaunti, lakini katika Serikali hii hilo ni ndoto,” alisema mama huyo
mkazi wa Kingorani.
Alidai watu kadhaa katika kaunti hiyo ambao hakuwataja, walibeba viti kisha baadaye wanamlaumu Katana.
“Kiti anachokalia Katana ni moto sana, joto la siasa limejaa, siasa si
uadui jamani. Tutatembea uchi mpaka kieleweke, iwe mara ya mwisho mama
yetu kudhulumiwa,” aliongeza Fatuma Atemi.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kaunti hiyo, Richard Chacha, alisema suala hilo linachunguzwa na vyombo vya usalama.
0 comments:
POST A COMMENT