
WAZIRI wa Mambo ya Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amesema
Serikali haiwezi kuona Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS)
kinajiingiza katika siasa.
Alisema kama wanataka hivyo, basi Serikali haitasita kuifuta Sheria ya TLS Sura ya 307 iliyoanzisha chama hicho cha wanasheria.
Dk Mwakyembe alikuwa akizungumza hayo na wageni wa TLS, waliomtembelea
ofisini kwake mjini Dodoma jana, wakiongozwa na Rais wa chama hicho
anayemaliza muda wake, John Seka.
“Kama wizara hatujui mwelekeo wa TLS kwa sasa, hatuwezi kuiacha TLS
ikijiingiza katika siasa halafu tukawaangalia tu. Hatuna nia ya
kuitawala TLS, ila tunawajibika kuwasimamia kwa kuwa Sheria yenu iko
chini yetu, mkiharibu kwa lolote wizara ndio yenye wajibu wa kuwatolea
maelezo katika hilo mnalotaka kulifanya sasa kuna mgongano wa maslahi,
je, ninyi kama wanasheria hamkuliona au hamlioni?” Alihoji Mwakyembe.
Wagombea wa TLS Mmoja wa wanasiasa wanaowania urais wa TLS ni Mbunge wa
Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye juzi alisema kitendo cha kukamatwa
baada ya kufutiwa kesi, kina nia ya kufifisha harakati zake za kuwania
urais wa TLS wiki ijayo, huku akitishia kugoma kula, endapo hatapelekwa
mahakamani mapema.
Lissu ambaye ni mbunge kwa tiketi ya Chadema, alikuwa na kesi katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akituhumiwa kutumia
lugha ya uchochezi katika kampeni za uchaguzi Jimbo la Dimani, Zanzibar.
Mbali na Lissu, wagombea wengine wanaowania nafasi hiyo inayoshikiliwa
na Rais wa sasa, John Seka ni kada wa Chadema, Lawrence Masha na
aliyewahi kuwa rais wa chama hicho mwaka 2011 hadi 2013, Francis Stolla.
Wengine ni Godwin Mwapongo na Victoria Mandari. Uchaguzi wa chama hicho
unatarajia kufanyika Machi 18, mwaka huu na mawakili 6,000 watapiga kura
kumchagua Rais mpya wa TLS.
Ufafanuzi wa Mwakyembe Alisema Serikali haina shida na wanachama wa TLS
kuwa wanachama wa vyama vya siasa ila ni lazima wafahamu kwamba viongozi
wanaowachagua ambao ndio watakaobeba sura ya TLS na mwelekeo mzima wa
chama kama wanataaluma hawapaswi kuwa na nasaba za kisiasa ili kuepusha
mgongano wa maslahi unapoweza kujitokeza.
“Serikali haina shida na wanachama wa TLS kuwa wanachama wa vyama vya
siasa ila tatizo linakuja pale mnapotaka kuchagua viongozi ambao tayari
wanazo kofia mbalimbali za uongozi ndani ya vyama vya siasa,” alisema na
kuongeza: “Hao ndio watakaobeba sura na mtazamo au mwelekeo wenu hapo
hatuwezi kukubali kwa kuwa watatenganishaje uongozi wao katika chama
husika na uongozi wao ndani ya TLS, huo sasa ndio mgongano wa maslahi.
“Ndio maana mwanasheria yeyote akiingia katika utumishi wa umma uwakili
wa kujitegemea anauweka pembeni ili kuepuka mgongano wa maslahi.”
TLS sasa imekua na haihitaji muangalizi kama ilivyokuwa miaka ya nyuma
nchi ilipopata uhuru, kwani ina wasomi wengi na vijana wengi wamekuwa
wanachama pia na kwa hiyo ni bora tuifute hii Sheria yenu na tuwape
mwanya mkajisajili kama NGO ambako kiongozi yeyote wa chama cha siasa
anaweza kuwa kiongozi wao,” alisema.
Aliwataka wafahamu kuwa dhamira ya Serikali ni njema huku ikizingatiwa
kwamba sheria kama zilivyo taaluma nyingine nchini, bado zinahitaji
uangalizi hasa ukizingatia uingiaji wa nchi katika utengamano wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Mkuu wa Wizara, Profesa Sifuni
Mchome alisema kila taaluma ina namna ya uangalizi wake. Alisema kama
wanasheria lazima kuhakikisha hatutoi vipaumbele kwa siasa, kama zilivyo
fani nyingine nchini.
Alitaka wajiulize kama kweli hawauoni mgongano wa maslahi, huku
wakizingatia kuwa wanapaswa kuhudumia jamii ya watanzania bila ya
kuwabagua.
“Kama wanasheria lazima tuhakikishe hatutoi vipaumbele kwa siasa kama
zilivyo fani nyingine, jiulizeni kama kweli hamlioni jambo hilo kama ni
kikwazo huku mkizingatia kuwa tunatakiwa kuhudumia jamii bila ya
kuwabagua sasa tukijiingiza katika siasa tutaihudumiaje jamii husika?
TLS kutojihusisha na siasa ni miongoni mwa kanuni za kutuimarisha kama
wanataaluma,” alisema Profesa Mchome.
Alisema Wizara ipo kuiangaliaTLS, na ndicho ilichofanya.
“Tupo hapa kuwaangalia, na ndicho tulichofanya, tumewashtua jamani
mnaenda wapi? Hatuna nia mbaya ila tunawataka muwe katika mstari, hivi
kweli kamati ya uchaguzi haijaona kama kuna mgongano wa maslahi hapo?
Alisema Serikali haitasita kuchukua hatua ya kuifuta Sheria ya TLS, kama
chama hicho kitaendelea na msimamo wa kujihusisha na masuala ya siasa
au kiuharakati.
Alisema chama hicho hakina budi kuangalia namna kinavyoweza kujikwamua katika hilo.
Kama hamuwezi kuendeleza misingi ya kitaaluma ya kutojihusisha na siasa
au vyama vya siasa, basi serikali haitakuwa na namna zaidi ya kuifuta
sheria ya TLS na TLS ya sasa itabidi ikajisajili kama NGO ili iendeleze
harakati zake; na Serikali itaunda sheria nyingine itakayoanzisha chombo
kitakachosimamia misingi ya kitaaluma.
0 comments:
POST A COMMENT