Kwa nini mazoezi ni muhimu katika kuzuia na kuudhibiti ugonjwa wa kisukari?
Jumatatu ya tarehe 14 Novemba ilikuwa ni siku ya KISUKARI duniani. Ujumbe wa mwaka huu ulikuwa ukisisitiza macho yote kuelekezwa katika
kuutizama ugonjwa huu unaonekana kuongezeka kwa kasi sana katika Jamii
ya waTanzania. Kikubwa kilichosisitizwa ni umuhimu wa kupima ili kuweza
kuchukua hatua madhubuti mapema.
Wengi wetu tayari tunafahamu ukweli kwamba kutokufanya mazoezi
kunachangia kwa kiasi kikubwa sana katika kusababisha ugonjwa huu.
Lakini huenda bado haijatuingia akilini ni jinsi gani mazoezi huweza
kusaidia katika kuzuia na hata kudhibiti sukari kupanda kwa watu ambao
tayari wana ugonjwa wa kisukari.
Leo tutajadili sababu kubwa tatu zinazofanya mazoezi kuwa moja wapo ya tiba na kinga ya ugonjwa wa kisukari.
MAZOEZI HUSAIDIA KUPUNGUZA MAFUTA MWILINI
Moja wapo ya vitu vinvyochangia katika kusababisha ugonjwa wa kisukari aina ya pili (type 2 diabetes) ni ongezeko la mafuta mwilini.
Mafuta yanapoongezeka mwilini huzifanya chembe hai za misuli kushindwa
kutumia homoni ya insulin vizuri. Homoni ya insulin ndiyo kichocheo
muhimu kinachosaidia sukari kuweza kutumika kutengeneza nguvu mwilini.
Kushindwa kwa misuli na viungo vingine kuitumia homoni hii, husababisha
sukari kubaki kwenye damu hivyo kuongezeka na kusababisha kisukari au
kuleta madhara kwa wale ambao tayari wana ugonjwa huo.
Kufanya mazoezi husaidia kupunguza mafuta mwilini hivyo kuifanya homoni ya insulin kufanya kazi kwa ufanisi. Kwa kufanya hivyo sukari huweza kutumika ipasavyo katika kutengeneza nguvu mwilini. Kwa maana hiyo inakuwa haibaki katika damu.
MAZOEZI HUSAIDIA MISULI KUTUMIA SUKARI
Katika
hali ya kawaida, asilimia zaidi ya 70 ya sukari inayopatikana katika
chakula hupelekwa katika misuli (skeletal muscle) mara tu baada ya mlo.
Hii ina maana kwamba ufanyaji kazi wa misuli ni muhimu sana katika
kuifanya sukari itumike mwilini. Misuli huweza kutumia sukari kwa
kupitia njia mbili tofauti. Ile inayohitaji insulin (insulin dependent
pathway) na ile isiyohitaji insulin ambayo husababishwa na mazoezi
(non-insulin dependent pathway). Kwa mgonjwa wa kisukari, kutokana na
ukweli kwamba insulin haifanyi kazi vizuri, ina maana kwamba kutumia
sukari kwa njia inayotegemea insulin hakufanyi kazi. Kwa maana hiyo
basi, njia pekee inayokuwa imebaki ni ile ya kutumia mazoezi.
Kwa lugha rahisi ni kwamba, wakati
njia ya kutumia sukari kwa kutegemea insulin haifanyi kazi kwa mgonjwa
wa kisukari, njia inayosababishwa na mazoezi huwa njia mbadala
inayouwezesha mwili wa mtu mwenye kisukari kuweza kutumia sukari, licha
ya insulin yake kutokufanya kazi vizuri.
Kwa maana hiyo kufanya mazoezi ni muhimu sana kwa mgonjwa wa kisukari aina ya pili (type 2 diabetes) maana hii humpa fursa ya mwili wake kuweza kuitumia sukari inayotoka katika chakula, hivyo kuzuia isiongezeke katika damu.
MAZOEZI HUSAIDIA KUONDOA MSONGO WA MAWAZO
Tafiti zinaonyesha kwamba msongo wa mawazo
wa kupitiliza huweza pia kuchangia katika kusababisha magonjwa sugu
kama kisukari. Hii inatokana na ukweli kwamba msongo wa mawazo au stress
husababisha ongezeko la muda mrefu la homoni inayoitwa cortisol. Homoni
hii hujuliakana kama homoni ya msongo wa mawazo (stress hormone).
Kuongezeka kwa kichocheo cha msongo wa mawazo (cortisol) kwa muda mfupi ni muhimu, kwani hutusaidia kuweza kufanya kazi na kutimiza majukumu. Bila stress kidogo tusingeweza kutimiza majukumu.
Tatizo
ni pale homoni hii inapokuwa imeongezeka kwa muda mrefu. Kuongezeka
huku kwa muda mrefu husababisha homoni ya insulin kutokufanya kazi
ipasavyo (insulin resistance) kitu ambacho husababisha ugonjwa wa
kisukari aina ya pili. Mazoezi ya mara kwa mara husaidia kuzuia
kuongezeka kwa muda mrefu kwa homoni ya cortisol, kitu ambacho huifanya
homoni ya insulin kufanya kazi vizuri. Homoni ya insulin inapofanya kazi
vizuri sukari hutumika ipasavyo hivyo kutokuongezeka katika damu.
HITIMISHO
Mazoezi
ni zaidi ya kupunguza mafuta na kuzuia unene. Hakikisha unajenga tabia
ya kufanya mazoezi mara kwa mara bila kujali kama wewe ni mnene au
mwembamba.
0 comments:
POST A COMMENT