Mama
mjamzito anapokunywa pombe, pombe huenda kwa mtoto kupitia kwenye kondo
(placenta), kisha kwenye mrija wa kitovu na hatimaye kwenye mzunguko wa
damu wa mtoto aliyeko tumboni.
Kwa kuwa mtoto aliyeko tumboni bado viungo vyake havijakomaa vizuri, anakuwa hana uwezo wa kumeng’enya (metabolize) pombe kwa haraka kama ilivyo kwa mtu mzima na hivyo huwa na kiwango kikubwa cha pombe kwa muda mrefu.
Nini madhara ya kutumia pombe wakati wa ujauzito
Kisayansi hakuna kiwango chochote cha pombe kilichoonekana kuwa salama kwa mama mjamzito.
Tafiti zimeonyesha hata wanawake wanaokunywa kiasi kidogo cha pombe
wanahatarisha maisha ya watoto wao. Utumiaji wa pombe wakati wa ujauzito
umehusishwa na madhara kadhaa yakiwemo yale yanayotokea mara mtoto
anapozaliwa na mengine hutokea baadaye watoto wanapokuwa watu wazima.
Ugonjwa wa pombe kwa mtoto (Fetal Alcohol Syndrome)
Dalili za tatizo hili huonekana mara mtoto anapozaliwa na hizi ni pamoja na
- Kuzaliwa na uzito mdogo na kichwa kidogo
- Ukuaji hafifu
- Kuwa na macho madogo, na kope zilizolegea
- Kuwa na pua ndogo
- Kuwa na taya dogo
- Kuwa na midomo ya juu myembamba
- Matatizo ya mfumo wa fahamu ambayo ni pamoja na; utindio wa ubongo, kuchelewa kukaa, kutambaa, kutembea, kuchelewa kuongea na kupata degedege.
Madhara yanayotokea baadaye
Pamoja
na madhara ya ugonjwa wa pombe yanayotokea mara baada ya kuzaliwa kwa
mtoto, yapo pia mengine ambayo hutokea mtoto anapokuwa mkubwa, na haya
ni pamoja na
- Matatizo ya akili yakiwemo ya sonona na kichaa (psychosis)
- Matatizo ya shule; utoro, kukosa nidhamu, kutokuwa na utii
- Uvunjaji wa sheri; kuwa na hasira sana, kushiriki kwenye ugomvi mara kwa mara
- Matatizo ya ulevi wa kupindukia na utumiaji wa madawa ya kulevya
- Kushindwa kufanya kazi kwa kujitegemea na kupoteza kazi mara kwa mara.
Mambo ya kufanya kuepukana na madhara haya
Mambo ya muhimu ya kuzingatia ili kumkinga mwanao na athari za pombe
- Hakikisha unaacha kunywa pombe kabisa wakati unajiandaa kubeba ujauzito
- Pombe aina zote ni hatari kwa afya ya mtoto
- Ni vizuri kwa akina baba kuacha pia pombe ili kuwawezesha wenzi wao kuepuka pombe kwa urahisi. Hata hivyo hakuna uhusiano wowote wa matumizi ya pombe kwa akina baba na matatizo ya pombe kwa mimba.
CHUKUA TAHADHARI SASA
0 comments:
POST A COMMENT