MWANAMUZIKI Chris Brown ni miongoni mwa mastaa waliojizolea umaarufu
mkubwa kutokana na maisha yao ya kila siku kutawaliwa na vituko.
Kwa sasa supastaa huyo anatajwa kuwa na matatizo ya akili tangu
alipotemwa na meneja wake. Matatizo hayo yanatajwa kuchangiwa na utumizi
wa dawa za kulevya.
Meneja Mike Guirguis aliachana na Chris mwaka jana huku akidai kudundwa na mwimbaji huyo na kulazimika kulazwa hospitali.
Kwa mujibu wa taarifa ya gazeti la New York Daily News, Mike G, alidai
Chris alimwalika nyumbani kwake na ghafla alianza kumshambulia kwa ngumi
nzito.
Itakumbukwa hata alipomshambulia kwa makonde aliyekuwa mpenzi wake,
Rihanna, mwaka 2009, Chris alitajwa kuwa alikuwa ametumia dawa za
kulevya.
Siku chache baada ya tukio hilo, Chris alikiri kuhudhuria ‘rehab’. Pia,
ilisemekana kuwa kuachana na Karrueche Tran kulitokana na sababu hiyo.
Lakini sasa, baada ya Mike G kujiweka kando na shughuli zote zinazomhusu
Chris, imeelezwa kuwa hali ni mbaya kwa mkali huyo kwani ameongeza
‘dozi’ ya dawa za kulevya.
Taarifa zimedai Chris hayuko sawa na amekuwa akitumia dawa za kulevya
kwa kiasi kikubwa, jambo linalotishia hatima ya maisha na kazi yake ya
muziki.
Mmoja kati ya walinzi wake wa karibu alisema: “Baada ya kumfanyia vile Mike G, kila kitu kiliharibika.”
“Hatukuwa na meneja wa kutuambia cha kufanya na wapi tunaelekea. (Chris)
akikasirika, anaweza kuwaambia watu walale kwenye gari (badala ya
hotelini). Alikuwa akiwatisha watu na polisi. Alikuwa akijiita shetani.”
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari za burudani, idadi kubwa ya wafanyakazi wake wameshamkimbia Chris.
Miongoni mwao ni aliyekuwa msimamizi wa ziara za kimuziki za staa huyo, Nancy Ghosh, ambaye alidai Chris alitishia kumpiga.
Mtaalamu wake wa matangazo, Nicole Perna, naye alikimbia kibarua kwa
madai kuwa bosi wake huyo alimkashifu kwa madai kuwa alishindwa
kutangaza kampuni yake ya mavazi ya Black Pyramid.
Lakini pia, hata marafiki wa karibu wa Chris wamekuwa wakiogopa kumsogelea mshikaji wao huyo kutokana na hali yake ya sasa.
“Huwezi kuzungumza na ‘mteja’, mtu ambaye hayuko sawa. Haingii akilini,” alisema mmoja wa marafiki zake.
“Ni jambo unalotakiwa kulifanyia kazi. Unatakiwa kubadili mfumo wako wa
maisha. Hafanyi kile kinachopaswa kufanyika ili kurejea katika uzima,
hivyo hawezi kuwa sawa.”
Kwa sasa watu pekee waliobaki karibu na Chris wanatajwa kuwa ni ndugu zake wa damu akiwamo mama yake mzazi.
Kwa wasiomfahamu, jina lake halisi ni Christopher Maurice “Chris” Brown
na alizaliwa Mei 5, 1989. Ngoma yake ya kwanza ni ‘Run It!’ ambayo
ilishika nafasi ya kwanza kwenye chati za Billboard.
0 comments:
POST A COMMENT