Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda anatarajiwa kuwa mgeni rasmi
katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yanayotarajiwa kufanyika
Machi 8 Mwaka huu, katika uwanja wa Mwembeyanga Temeke Jijini Dar es
Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam jana maadhimisho hayo yataongozwa na maandamano ya Wanawake na
wadau mbalimbali, na yataanzia katika Shule ya Msingi Mabatini kuelekea
viwanja vya Mwembeyanga.
Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Mwaka huu yanaongozwa na kauli
mbiu isemayo “Tanzania ya viwanda, Wanawake ndio Msingi wa Mabadiliko ya
Kiuchumi”.
Kauli mbiu hiyo inalenga kuikumbusha jamii kuhusu umuhimu wa kujenga
mazingira wezeshi kwa Wanawake hasa kutambua mchango wao katika kuleta
Maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla.
Taarifa hiyo pia imeikumbusha jamii kuhusu wajibu wake ikiwa ni pamoja
na kuwashirikisha, kuwaamini na kuwapa Wanawake haki sawa katika nafasi
za Elimu, Uchumi na uongozi ili wawe chachu ya mabadiliko yenye lengo la
kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
Maadhimisho hayo yataambatana na maonesho ya kazi za ujasiriamali
yanayoendelea katika uwanja wa Mwembeyanga, ambapo Asasi za kiraia na
vikundi mbalimbali vya wanawake vitaonesha bidhaa zao.
Aidha, Wananchi wa Mkoa wa Dar es salaam wanakumbushwa kushiriki kwa
wingi katika maadhimisho hayo ikiwa ni pamoja na kuwa na mikakati ya
kukabiliana na changamoto mbalimbali zinanazowakabili Wanawake kuanzia
ngazi ya kaya hadi Taifa.
0 comments:
POST A COMMENT